Vilio vyetu sote, wachache wanacheka,
Bahati si nzuri, hakuna wa kusikia,
Vilio na vicheko…vyote ni kelele,
Nani akusikie, au nani akujali?
Kusikia tunasikia pasi na kuelewa,
Kuwahi ni ugonjwa, yetu sifa kuchelewa,
Nani hufurahi, bintiye kuchezewa?
Lakini…
Taifa hili changa, kipi kigumu kupanga?
Utajiri umejaa hauhesabiki kama mchanga,
Tugawane kwa haki jamani bila ncha ya upanga!!
Maji tunayo kwanini tukabwe na karanga?
Nataka mdundiko iweje unipigie charanga?
Hii ni tamu, hii ni chungu,
Shida zimejaa twagawana kwa mafungu,
Tumwage damu, tushike rungu,
Basi chini tunakaa, yote ataamua mungu.
Ndiyo, labda tumwachie mungu aliyetuumba,
Maana ni “genius” yule jamaa aliyetufumba,
Anadai kutusimulia, huku anaongeza sauti ya rhumba,
Si wizi au ubepari, ni nguvu ya maendeleo hii kasumba…
Mchumia juani hulia kivulini,
Ha ha!! Haiingii puani wala akilini,
Kwani vya juani vimekauka, na kivulini wameshajaa,
Kwa subira tumenyauka, ahadi hazijatufaa,
Kama nyani tumepauka, wahanga wa sanaa…
Ndiyo wasanii hawajang’atuka, wamejawa na tamaa..
Utotoni tuliambiwa mkubwa hakosei,
Au ndiyo kusema mchora ramani hapotei?
Sidhani, ni sawa kama alichoahidi hakitokei…
Na hiko “kidogo” upatacho, mbona hatushei?
Watuacha tunakonda, mbeletu wafunga mlango,
Moyoni ni vidonda, watunyima japo robo ya mpango,
Hii ni tamu, hii ni chungu,
Shida zimejaa twagawana kwa mafungu,
Tumwage damu, tushike rungu,
Basi chini tunakaa, yote ataamua mungu.
Kuna maswali mengi najiuliza na roho yangu mkononi…
Hivi ni kweli mbio za sakafuni huishia ukingoni?
Maana sakafuni wanakimbia na bado wana tabasamu midomoni,
Wenzangu na mie, tumesimama tukisubiri mpaka manundu migongoni…
Miye na Juma, upwa tumegaa nao na bado wali mkavu,
Kumbe hata ukiona samaki, kumwokota ni ubavu!!?
Ole wetu serikali ikiweka kodi ya watu na uchakavu!!
Msicheke, maana nyundo hii ni nzito,
Wenzenu tumebeba mibuyu, heri wenu wa fito,
Lakini kumbukeni, dunia mapito…
Kinachouma, nikipata moja mwenye mia tayari kafika,
“Cheza Bahati nasibu” …utabahatika…
Ooh “weka kwenye saccos yangu” utahamasika…
Wiki mbili baadaye kote patashika…
Ofisi ya miaka kumi inapotea kwa dakika…
Sisi wenye moja zetu, nani tumfinye kwa hakika?
Hii ni tamu, hii ni chungu,
Shida zimejaa twagawana kwa mafungu,
Tumwage damu, tushike rungu?
Basi chini tunakaa, yote ataamua mungu.
Maneno hayaniishi, kidooogo nyuma ya machungu,
Kwenye bendera kuna rangi yangu na si ya mzungu,
Lakini kuna sehemu, mwenzangu yeye mungu,
Eti maji ya chupa hayachanganywi na ya chungu!!?
Jibu silijui lakini utaifa mi nnao…
Japo ni haki yangu nashangaa hata kusikika ni kwa mgao,
Sauti zinazibwa, eti “top secret” kila kikao…
Watu wasiulize, wamevuka mipaka ya uhuru wa kujieleza,
Wewe ni nani ambaye hukosei na kuteleza?
Uhuru tunao, wa kusema baada ya kupeleleza,
Tukiomba majibu kwanini tusipewe ya kutosheleza?
Wenzangu, wakina “tia mchuzi pangu pakavu” ni wengi,
Tukicheka na kusubiri watukumbuke, taifa hatujengi,
Kwa maneno na ahadi kwa kweli hawatutengi,
Ila… lile fungu la kupata, haswa halitulengi,
Ahadi zilikotoka huko huko zinarudi,
Wewe mtanzania, kusimama na kudai huna budi,
Bila juhudi, wote tutakuwa majambazi kama masudi,
Nani atamkimbia nani, maana wote wezi,
Wewe umeiba Prado mimi nina benzi,
Nani anyooshe kidole na wizi kwetu mapenzi?
Dini tumeianzisha, na juu ya haki tumeiweka kwa enzi..
Haki yetu imekuwa tamu chungu,
Shida zimetujaa, ni kweli tumuachie mungu?
By, Khery Mbiro “the poet” © 2009, June 26th.